Head image
Govt. Logo

Hits 115687 |  2 online

           


SERA YA MAZINGIRA NI MAISHA YA KILA MTU
news phpto

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akizinduwa Mchakato wa Mapitio ya Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya Mwaka 2013, huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa Mamlaka husika Nchini kuhakikisha Mapitio ya Sera ya Mazingira yanakuwa shirikishi katika ngazi zote, kwa kuzingatia kwamba maisha ya kila siku ya Wananchi yanategemea maliasili.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo wakati wa Uzinduzi wa Mchakato wa Mapitio ya Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya Mwaka 2013, huko katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.

Amesema, Zanzibar hivi sasa inashuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi na ya kijamii yanayopelekea matumizi makubwa ya maliasili ziliopo, ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa, kuongeza shinikizo katika ikolojia za baharini na nchi-kavu, na kinachodhihiri ni kuwa Mabadiliko ya Sera ya Mazingira yanahitajika ili kwenda sambamba na kukabiliana na changamoto za kimazingira, ili hatimaye kuielekeza Nchi na Taifa kwa ujumla, katika maendeleo endelevu, yanayozingatia matumizi bora ya maliasili ziliopo, za nchi-kavu na baharini.

“Kwa ajili ya kufikia kwenye azma hiyo, ni vyema Mchakato wetu wa Kupata Sera Mpya ya Mazingira uwe shirikishi katika ngazi zote, ili pia kupata maoni kamili ya wadau juu ya mambo muhimu na ya msingi, ambayo yanafaa kuzingatiwa kwenye Sera hiyo, pamoja na kuelewa ni upi wajibu wa wadau katika kuhakikisha utekelezaji wake”, amesisitiza Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman ameeleza kuwa Miaka 10 imepita tokea kuzinduliwa kwa Sera ya Mazingira ya Mwaka 2013, ambapo tangu Mwaka 2013, kumekuwepo na Maamuzi kadhaa ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa yanayoelekeza Visiwa vya Zanzibar kufikia Lengo la Maendeleo Endelevu, ambayo ni pamoja na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050; Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa 2021-2026; Mpango wa Kuirithisha Zanzibar ya Kijani (Zanzibar Green Legacy Programme), kwa azma pia ya kusimamia utekelezaji wa Mikataba, Maazimio na Makubaliano ya Kimataifa juu ya Usimamizi wa Mazingira, ambapo pia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia na au imesaini pamoja na kuwepo kwa Sera nyengine Mpya za Kisekta, ikiwemo Sera ya Uchumi wa Buluu 2022.

“Kama mnavyofahamu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Idara ya Mazingira inalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa nyezo za usimamizi wa mazingira ambazo ni pamoja na Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati na Miongozo ya kimazingira, zinakuwepo na kutekelezwa kikamilifu, ili kusaidia katika usimamizi bora na endelevu wa mazingira hapa Visiwani; kutokana na majukumu hayo, mnamo Mwaka 2013 Sera ya Mazingira iliandaliwa ili kuchukua nafasi ya Sera iliyoitangulia ya Mwaka 1992; Sera hii ilihusisha Sekta mbalimbali zikiwemo Maji, Afya, Misitu, Utalii, Kilimo, Ufugaji, Nishati, Uvuvi na Rasilimali za Baharini kwa ujumla”, amefafanua Mheshimiwa Othman.

Amefahamisha kuwa Zanzibar katika hali yake ya asili ilikuwa na mazingira mazuri, yenye fukwe za kupendeza, bahari iliyosheheni rasilimali za aina tofauti, udongo wenye rutuba, miti na wanyama wa aina mbalimbali, mambo ambayo yalipelekea kuifikisha Nchi katika maendeleo yaliyopo sasa.

Hata hivyo amesema, hali hiyo kwasasa imeanza kubadilika na kuleta changamoto kadhaa za kimazingira ambazo zimeshajitokeza na kuwa tishio kwa mustakabali wa maendeleo endelevu ya Nchi na Taifa kwa ujumla.

Hivyo ameagiza kwa kusema, “tunapaswa kuhakikisha kwamba, Mchakato wa Mapitio ya Sera ya Mazingira unatuhakikishia kuwa tunakuja na Sera Mpya ya Mazingira ambayo inatuvusha hapa tulipo na kuiweka Zanzibar kwenye ramani ya dunia, ikiwa na mazingira bora na endelevu kwa faida ya kizazi cha leo na kijacho”.

Mheshimiwa Othman amefahamisha kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, pamoja na Serikali kwa jumla, inategemea kupata Sera ya Mpya ya Mazingira ambayo ni shirikishi, iliyo bora kabisa, na yenye kutekelezeka, kwaajili ya maendeleo endelevu ya Zanzibar. Sekta ya Mazingira, na kwa kuzingatia kwamba yenyewe ni “Sera Mtambuka”.

Aidha Mheshimiwa Othman ameishukuru kwa dhati Taasisi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania, kwa msaada wa kitaalamu na wa kifedha kwaajili ya kuwezesha mapitio ya Sera hiyo, ambapo amesema mategemeo yaliyopo ni pamoja na kuwa Wataalamu hao wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, katika kutayarisha Mpango wa Utekelezaji wa Sera na pia maeneo mengine muhimu ya mabadiliko ya tabianchi.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Bi. Harusi Said Suleiman, ameshukuru juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi nyengine, ili kutimiza lengo la kupambana na athari za mazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akieleza Lengo Kuu la Mkutano huo ambalo ni Kuzindua Mapitio ya Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya Mwaka 2013 ili kupata Sera ya Mpya ya Mazingira kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Omar Dadi Shajak, ameitaja dhamira ya Hatua hiyo akisema, “Sera ya Mazingira ya Mwaka 2013 imekuwa ikituongoza kwa takriban miaka 10, na sasa kwa kushirikiana na Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, tunaanza mchakato wa kuifanyia mapitio na maboresho, ili hatimaye kupata Sera yenye kubeba maono mapana ya Sekta ya Mazingira, ambayo ni miongoni mwa Sekta Mtambuka”.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Climate Action Network (CAN) Tanzania, Dokta Sixbert Mwanga, ameeleza kwamba Taasisi yake inafanyakazi kwa kutarajia mabadiliko endelevu katika ngazi zote, kupitia nadharia ya 'Think' ambayo inalenga katika Sera, Ubunifu na Miongozo ya Kisekta; sambamba na 'Tank' inayoangaza dhamira ya utekelezaji wa vitendo katika nyanja zote za maisha ya watu ndani ya Jamii, kwa uhalisia na upana wake.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wadau wa Mazingira, Washirika wa Maendeleo na Asasi za Kiraia wameshiriki katika Hafla hiyo wakiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar, Bw. Sheha Mjaja Juma; Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar, Madam Farhat Ali Mbarouk; Mrajis wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Bw. Ahmed Khalid Abdulla; Mwenyekiti wa Bodi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania, Dokta Catherine Massao; na Washiriki kutoka Wizara na Taasisi mbali mbali.

Mkutano huo wa Siku Moja, ambao umekijumuisha pia Kikosi-Kazi cha Kuandaa Sera Mpya ya Mazingira, umeandaliwa na Taasisi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania yenye Makao yake Makuu Jijini Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe Waziri



Tel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz