Head image
Govt. Logo

Hits 115689 |  2 online

           


UGAWAJI WA VIFAA VISAIDIZI KWA WATU WENYE ULEMAVU.
news phpto

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman alievaa mtandio mwekundu pamoja na baadhi ya viongozi wa BLTWW na UWZ amekabidhi vifaa visaidizi kwa Watu wenye Ulemavu vilivyotolewa na taasisi ya Wheel to Heel kutoka Uingereza kwenye ukumbi wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu uliopo Kikwajuni, Wilaya ya Mjini,Unguja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe Harusi Said Suleiman ameishukuru taasisi ya Wheel to Heel ya Uingereza kwa jitihada na michango mbali mbali wanayoitoa kwa Watu wenye Ulemavu.

Mhe Harusi aliyasema hayo wakati akikabidhi vifaa visaidizi kwa Watu wenye Ulemavu ikiwemo viti vya magurudumu, magodoro, dawa, magongo ya kutembelea na pempas vilivyotolewa na kampuni ya Wheel to heel ya Uingereza.

Amesema msaada wa vifaa visaidizi vilivyotelewa na taasisi ya Wheel to Heel utasaidia katika kuondosha changamoto zinazowakabili Watu wenye Ulemavu waliobahatika kupata msaada huo wakati wakiwa katika maeneo mbali mbali na kwenye harakati zao za maisha.

Waziri Harusi amefahamisha na kuwasisitiza wote waliopatiwa msaada wa vifaaa visaidizi kuvitunza pamoja na kuthamini mchango uliotolewa kwa kuweka mahali salama kuepuka kuharibika au kuvunjika kwa vifaa hivyo ili viweze kudumu.

Mhe. Harusi amewasihi Watu wenye Ulemavu kujikinga na maambukizi ya UKIMWI, pia kutokubali kushawishiwa kujiingiza kwenye biashara haramu ya dawa za kulevya na hivyo wanapaswa kupaza sauti zao na kupinga vikali uwepo wa biashara hiyo ambayo imekua ikiathiri dunia na vizazi vyake.

Sambamba na hayo,Mhe Harusi amewakumbusha Watu wenye Ulemavu kuendelea kudumisha amani ya nchi na kutokubali kushirikishwa katika vitendo vinavyosababisha kuvunjika kwa amani ya nchi kwani nao wanao wajibu wa kuihamasisha jamii kujiepusha na vitendo viovu vinavyohatarisha maisha yao na jamii kwa ujumla.

“Ombi langu kwenu ndugu zangu wenye ulemavu tusikubali kushawishiwa kuiondosha amani iliyopo katika nchi yetu,tufahamu kwamba endapo amani itatoweka watu wa mwanzo kuathirika ni Watu wenye Ulemavu,”alisema

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu, Mhandisi Ussy Khamis Debe amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ina azma ya kuhakikisha kuwa Watu wenye Ulemavu wanaendelea kuwa katika jamii jumuishi.

Amesema Serikali kupitia Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu itahahakikisha haki za Watu wenye Ulemavu zinalindwa pamoja na kuwatafutia mbinu mbadala za kujikwamua kiuchumi na kuwapatia vifaa visaidizi kila hali inaporuhusu kwa kushirikiana na wafadhili na wote wanaojitolea kusaidia juhudi hizo.

Nae,kiongozi mkuu wa taasisi ya Wheels to Heel ya nchini Uingereza, Khalid Raza amesema wamefarijika kutokana na mashirikiano mazuri waliyoyapata kutoka Serikalini na kuahidi kuwa msaada walioutoa hautokua mwisho bali utakua endelevu.

“Tumeridhishwa na tumefurahi kuona msaada tulioutowa umefika kwa walengwa” alisema Raza

Akitoa shukurani kwa niaba ya wenzake mmoja wa waliopata msaada huo Amina Daud Simba alisema msaada walioupata utasaidia kuondokana na changamoto zinazowakabili na kuahidi kutumia vizuri vifaa visadizi pamoja na matumizi sahihi ya dawa walizopewa.

Amina alisema kutokana na kuuzwa bei vifaa visaidizi na hali ya maisha ya Watu wenye Ulemavu wanashindwa kununua hivyo kupatikana kwa vifaa visaidizi vitasaidia kuondosha baadhi ya changamoto zinazowakabili.

“Kwa niaba yangu na wenzangu tunatoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu kwa juhudi wanazozichukua katika kutusaidia,lakini pia tunaishukuru taasisi ya Wheel to Heel kwa kutujali na kuona umuhimu wa kuja kutusaidia,”alisema Amina.

Hafla ya kukabidhi vifaa visaidizi imefanyika kwenye ukumbi wa Watu wenye Ulemavu uliopo Kikwajuni, Wilaya ya Mjini ambapo vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 260 za kitanzania.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe Waziri



Tel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz