Head image
Govt. Logo

Hits 115662 |  1 online

           


TUNZENI MAZINGIRA KUIENZI ZANZIBAR
news phpto

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Nchi hii ilitambulika ulimwenguni kutokana na alama zake muhimu za kihistoria na mazingira bora ya kuvutia, ambayo yanahitaji kuendelezwa ili kukuza na kuendeleza heshima yake.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Nchi hii ilitambulika ulimwenguni kutokana na alama zake muhimu za kihistoria na mazingira bora ya kuvutia, ambayo yanahitaji kuendelezwa ili kukuza na kuendeleza heshima yake.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika ziara yake ndani ya Wilaya tatu za Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, akiangalia athari za kimazingira kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema licha ya Zanzibar kujengeka vyema na maumbile bora ya visiwa vyake, bali uzuri wa mazingira ya kuvutia, mandhari tulivu ya asili, majengo na maeneo ya kihistoria, pamoja na mabustani, yalipelekea kuwa kivutio cha wageni kutembelea Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Othman ameeleza haja ya juhudi za pamoja kutoka sekta mbali mbali za serikali, jamii na taasisi binafsi, kuyaendeleza na kuyaokoa mazingira, ambayo kwa sasa yanakabiliwa na tishio kubwa la uharibifu sambamba na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kulinda na kurudisha hadhi na heshima ya Zanzibar ulimwenguni.

Aidha ametolea mfano Nchi za Malaysia na Ushelisheli, zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa kujiokoa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira na hatimaye kuyageuza maeneo mengi kuwa neema kupitia vivutio na uzalishaji.

Mheshimiwa Othman, katika ziara yake hiyo aliweza kuyatembelea maeneo mbali mbali yakiwemo mashamba yaliyovamiwa na maji ya bahari ya Chuini, Maporomoko ya Masingini, Kiwanda cha Chuma-chakavu Kisakasaka, Machimbo ya Kokoto ya Fumba, Bustani ya ‘Botanic’ Migombani, na mmomonyoko wa Ukuta wa Shangani-funguni, yote katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wakieleza changamoto zinazowakabili, baadhi ya wananchi wametaja ukosefu wa vifaa na usalama, mitaji, fedha taslim, kukosekana kwa wafadhili, ugumu wa upatikanaji wa vibali, uchafu, na adha kutokana na wanyama na raia wapinga-maendeleo, ambayo yanadhoofisha juhudi zao za kuyatunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waliopaza sauti zao miongoni mwa wananchi hao, mbele ya msafara wa Makamu wa Kwanza wa Rais, ni pamoja na Katibu wa Ushirika wa Kutunza Mazingira Chuini, Bw. Hamad Juma Omar, Mmiliki wa Kiwanda cha Chuma-chakavu cha ZANARAB, Bw. Ali Makame Issa, na Katibu wa Jumuiya ya Kutunza Mazingira ya Mnara wa Mbao, Bw. Kombo Juma Maalim, ambao kwa pamoja wameiomba serikali kuungamkono juhudi zao ili kuinusuru nchi kutokana na majanga ya kimazingira.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dkt Saada Mkuya Salum, amesema licha ya juhudi na azma njema ya Serikali katika kuungamkono juhudi za kuyalinda na kuyatunza mazingira, kuna haja ya wadau kujiandaa na kuziendea taasisi zinazohusika na fedha na uwezeshaji, ili kutumia fursa za misaada na mikopo, katika kutekeleza na kendeleza mipango na miradi yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mazingira, Bw. Sheha Mjaja, amesema tafiti mbali mbali zimekuwa zikibaini tishio kubwa la uharibifu wa mazingira na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, yanayohitaji hatua za haraka kupitia juhudi za pamoja za kisekta ili kuinusuru nchi kutokana na majanga yanayoweza kujitokeza, yakiwemo matetemeko ya ardhi.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Othman, aliongozana na viongozi mbali mbali wa Kiserikali na wa kijamii akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Omar Dadi Shajak, na Wakuu wa Wilaya za Mjini, Magharibi A na Magharibi B, Ndugu Rashid Simai Msaraka, Bi Suzan Peter Kunambi, na Bi Hamida Mussa Khamis.

Huduma za Tehama

Barua Pepe

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

ZEMA ZAC DDA IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 2808, Migombani, Zanzibar
Tel.: +255(24)2232474 Mhe Waziri



Tel.: +255 (24)2232475 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2232476
Email: info@omkr.go.tz