Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akiwa katika mazungumzo na ujumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ujumbe huo umeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu Wa Rais Mhe.Mhandisi Hamad Yussuf Masauni; tarehe 18 Disemba, 2024.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema mashirikiano mazuri kati ya SMT na SMZ yatasaidia kuondosha changamoto za kimazingira nchini.
Ameyasema hayo ,Disemba 18, 2024, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Migombani Unguja,wenye lengo la kujitambulisha pamoja na kupokea ushauri na mapendekezo kuhusu masuala ya Mazingira na Muungano.
Amesema kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia kutekelezeka misingi iliyojiwekea katika kuimarisha masuala ya mazingira na maeneo yenye mashirikiano kwa vile ni Ofisi zinazotegemeana na ambazo zimebeba dhamana ya Serikali na vizazi vijavyo, huku akitolea mifano ushirikiano wa Mamlaka za Usimamizi wa Mazingira nchini zikiwemo Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) kuengeza mashirikiano.
Amesema pamoja na kuwa NEMC ni taasisi tofauti lakini ndio inayosimamia masuala ya mazingira katika ushirikiano wa kimataifa na kuendesha masuala mengi hivyo amesisitiza kuangalia fursa muhimu zilizopo Zanzibar katika kutekeleza majukumu ya nchi kwa upande wa mazingira.
Akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya muungano pamoja na dira ya Taifa ,Mhe. Othman amezitaka Mamlaka husika kuwa wabunifu zaidi na wawazi ili kuhakikisha ndoto za maendeleo na matarajio ya makundi yote nchini yanafikiwa.
Nae, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema lengo la kukutana na Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na uongozi wake ni kushauriana, kupata miongozo na maelekezo ambayo yataimarisha na kuendeleza ushirikiano uliopo.
Amesema japokuwa suala la mazingira sio la muungano ila unapokuja suala la uwakilishi wananchi wa Zanzibar itategemea kama ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweza kushiriki mambo na fursa mbali mbali hivyo mipango thabiti inahitajika kwa maslahi ya nchi.
Ujio na utambulisho wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ,ambae ameongozana na Naibu Katibu Mkuu Muungano ndugu Abdalla Hassan Mitawi, Mkurugenzi masuala ya Muungano ndugu Juma Mohamed Salum, umetokana na mabadiliko ya mawaziri yaliyofanyika hivi karibuni yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan.