Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akiwa katika Kilele cha maadhimisho ya siku ya Watu wenye Ulemavu duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Gombani,Wilaya ya Chakechake,Mkoa wa Kusini Pemba; tarehe 03 Disemba 2024.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameihimiza Jamii kuzingatia haki kwa Watu wenye Ulemavu, ili kuwajengea Mazingira bora ya Kimaisha, na ili kutoa Fursa sawa kwa Wote katika kukuza, kuimarisha na kuleta Maendeleo, na hatimaye kujenga Uchumi wa Nchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo, Disemba 03, 2024, wakati akiwahutubia Wananchi, katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani, huko Viwanja vya Gombani ya Kale, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema, hatua hiyo ni muhimu kwaajili ya maendeleo ya Nchi, na inakwenda sambamba na Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu ambayo ni ‘Kukuza Uongozi wa Watu Wenye Ulemavu kwa Mustakbali Jumuishi na Endelevu’, na ambayo pia inahimiza haki na fursa sawa kwa Kundi hilo la jamii.
Aidha, Mheshimiwa Othman amesema, “Kaulimbiu hii inakwenda sambamba na Sheria ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Na. 8 ya Mwaka 2022; na pia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, wa Mwaka 2009, ambao Tanzania imeuridhia, kwa madhumuni ya kuutekeleza; na yote haya ni katika azma ya Serikali kuona kwamba hakuna anaeachwa-nyuma katika maendeleo”.
“Tunafahamu kwamba watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo za kushindwa kupata baadhi ya haki zao za msingi; hata hivyo Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbali mbali, itahakikisha inakabiliana nazo au kuziondoa kabisa, pamoja na kuzingatia upatikanaji wa haki hizo; na katika Ujumbe wa Mwaka huu, ambao umebeba Ajenda ya Ushiriki na Ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu, ili Kukuza Wigo wa Kundi hili katika Nafasi za Uongozi Nchini, tumeona Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatoa msukumo wa aina yake kwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika nafasi mbali mbali za kiuongozi”, amefahamisha Mheshimiwa Othman.
Akitaja mambo ambayo ni hatarishi kwa sasa hapa Nchini, na yanayochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la Watu wenye Ulemavu, Mheshimiwa Othman ametaja Wimbi kubwa la Ajali za Barabarani; pamoja na Magonjwa yasiyokuwa ya Kuambukiza.
Hata hivyo, Mheshimiwa Othman amewaasa Vijana Wanaotumia Vyombo vya Moto Nchini, wakiwemo Waendesha Boda Boda, kuwa makini na kuepuka ‘ku-chart’ pamoja na hadhari katika Matumizi-holela ya Simu, wakiwepo barabarani, ili kuepuka kusababisha ajali, na au ulemavu usiokuwa wa lazima.
Aidha Mheshimiwa Othman, akitoa shukurani kwa niaba ya Serikali, kwa Washirika mbali mbali wa Maendeleo, amewashukuru pia Wananchi ambao wamejitokeza kwa wingi katika Kilele cha Maadhimisho hayo, akisema kuwa hayo yote ni ishara ya umoja na upendo uliopo sasa, miongoni mwa Jamii za Watu wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Mara tu alipowasili katika Viwanja hivyo, Mheshimiwa Othman amepokea Maandamano ya Watu wenye Ulemavu, yakiongozwa na Kikosi cha Bendi ya Chipukizi; na pia ametembelea Banda la Maonyesho la Wajasiriamali, ili kujionea Bidhaa mbali mbali, zinazotengenezwa na Watu wenye Ulemavu, wa Unguja, Pemba na hata Tanzania Bara.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Bi. Harusi Said Suleiman, katika Salamu zake ambazo zimewasilishwa hapo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, amesema kunapokuwepo na Umoja na Mshikamano katika Jamii, kunatoa fursa muhimu kwa Viongozi Wakuu wa Nchi, ili kutekeleza Mipango na Miradi ya Maendeleo, ikiwemo ya kuwajengea mazingira bora, na kuwasaidia Watu wenye Ulemavu.
Mhe. Hamza amewahimiza Wananchi wa Zanzibar, akisema kila inapobidi kuwepo kwa Viongozi Wakuu wa Nchi, au Maadhimisho ya Kitaifa, Watu wajitokeze kwa wingi kujumuika nao, bila ya kujali Itikadi zao za Vyama, kwani Katiba ya Nchi imeshaweka Misingi kwa Wafuasi wa Imani tofauti za Kisiasa, kufanyakazi kwa pamoja, na hiyo ni njia muhimu ya kujenga Amani, Umoja na Mshikamano, kuelekea katika Maendeleo ya kweli.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ndugu Rashid Hadidi Rashid, akitoa Salamu za Mkoa wake, amesema kufanyika kwa Maadhimisho haya, ni faraja na fursa kubwa, Nchini na Duniani kote, katika kuongeza hamasa, uelewa na uwezeshaji wa kuwajali na kuwathamini Watu wenye Ulemavu, ndani ya Jamii zao, na kote Ulimewenguni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Bi. Salma Saadat, amesema wao ni Sehemu Muhimu ya Jamii, na licha ya kuridhishwa kwao na hatua mbali mbali za kuwasaidia, zinazochukuliwa na Serikali zote Mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, bali mahitaji yao kwa sasa ni kuandaliwa Miundombinu Rafiki Zaidi, na pia kuwekewa Mazingira Bora ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa hapo Mwakani, Nchini kote.
Katika Risala yao, iliyosomwa na Bw. Haroub Soud Mzee, kutoka Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), pamoja na kueleza Changamoto zinazowakabili, zikiwemo za Upungufu wa Vifaa-saidizi; na Mafanikio yao yakiwemo ya Ushiriki wao katika Miradi mbali mbali ya Maendeleo, Watu wenye Ulemavu Nchini, wameiomba Serikali kuandaa Mazingira Bora yatakayowapatia wepesi katika Maisha ya Kawaida, ambayo ni pamoja na Fursa za Uteuzi wa Nafasi za Uongozi; Sera na Sheria Rafiki kwao, hasa Wakati wa Chaguzi; na Kuwaongezea Fungu Maalum la Bajeti kwaajili ya wale Wenye Ulemavu Mkubwa, sambamba na kuzisaidia Familia zinazoishi katika Mazingira Magumu.